HUKU timu yake ikiwa imebakiza mechi saba za Ligi Kuu Bara msimu huu na leo ikiialika Tanzania Prisons, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, ametaja vitu vitatu ambavyo amekutana navyo kwa mara ya kwanza tangu aanze kucheza na kufundisha soka.
Djuma alitua nchini mwaka jana na kuwa msaidizi wa aliyekuwa Kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Omog, na sasa yuko katika nafasi hiyo akimsaidia Mfaransa, Pierre Lechantre.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio juzi, Djuma, alitaja kitu cha kwanza kilichomshangaza ni "mahaba makubwa" ambayo wanayo mashabiki wa soka Tanzania hasa wa klabu za Simba na Yanga.
Djuma alisema pia amefurahishwa na ushindani wa timu hizo kongwe nchini ambao unawafanya makocha wajipange kukabiliana na changamoto katika kila mechi ya ligi hiyo ya juu nchini.
Alisema kingine ni ushirikiano kutoka kwa wanachama na viongozi ambao wamekuwa wakitoa mawazo yao hata pale wanapokutana nje ya kazi.
"Yaani mapenzi ninayoyaona sikuwahi kuyaona huko nyuma, tangu nikiwa mchezaji mpaka sasa nimekuwa kocha, kuna wakati tunafikiria baadhi ya mechi ni ndogo na za kawaida, lakini presha ya wanachama inakuamsha na kukubadilisha mawazo, hii sikuwahi kuiona Rayon ingawa ina mashabiki wengi pia," alisema kocha huyo.
Aliongeza kuwa amekuwa mwepesi wa kusikiliza maoni na yale yanayofaa amekuwa akiyafanyia kazi kwa maslahi ya timu na hayuko tayari kuingiliwa majukumu yake.
"Kingine ninachokifurahia nimefanikiwa kurejesha uhusiano wa wachezaji na benchi la ufundi ambao haukuwapo wakati nafika, hii imesaidia kutufanya tushirikiane vema na sasa tunaongoza ligi na kuendelea kuwa kwenye mbio za ubingwa," aliongeza kocha huyo raia wa Burundi.
Simba inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa kuikaribisha Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na baada ya hapo itawasubiri watani zao, Yanga Aprili 29, mwaka huu. Timu hizo zitaingia zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1.
Chanzo: IPP Media