Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi ameteuliwa kuwa balozi wa Mbeya Tulia Marathon 2018 inayotarajia kufanyika Mei 6, mwaka huu kwenye Uwanja vya Sokoine jijini Mbeya.
Mbeya Tulia Marathon inaasisiwa na Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson na itajumuisha mbio za km 42, km 21, km 150 kukimbia na baiskeli na km 5 kwa vyuo vya ufundi na vyuo vikuu ambapo zitatolewa milioni 40 kwa washindi.
Kinara huyo wa ufungaji wa Ligi Kuu Bara, Okwi alisema ameshukuru kwa nafasi hiyo aliyopewa na kwamba atahakikisha anayatangaza vizuri mashindano hayo.
"Nilipoalikwa niliona kama nafasi nzuri katika kuwafikia watu wengi. Nimefurahi kushiriki katika Marathon na ni jambo zuri linalofanyika," alisema Okwi.
Mratibu na balozi wa Tulia Trust, Hassan Ngoma alisema wameamua kuongeza nguvu kwa kumleta Okwi kuwa balozi wa mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya tatu.
Alisema lengo ni kuhakikisha tamasha hilo linafana ambapo fedha zitakazopatikana kwa wadau watakaochangia zitatumika katika eneo la elimu na afya.
"Tunaamini Okwi ni kipenzi cha watu na kupitia yeye tunaweza kupata wachangiaji wengi zaidi na kutimiza lengo letu la kusaidia elimu na afya. Kwahiyo kupitia yeye tutahakikisha tamasha linafana," alisema Ngoma.
Alisema mpaka sasa mwitikio wa washiriki hao ni mkubwa na kwamba wanaendelea kupokea washiriki kutoka nchi mbalimbali.
Alitaja ada kwa washiriki kuwa ni Sh30,000 kwa washiriki wa mbio za km 42, Sh20,000 kwa km 21 na kukimbia na baiskeli na vingine Sh10,000 ambapo malipo yatatumwa kwa Tigopesa, Mpesa na Airtel Money.
Aliongeza kuwa mshindi wa kwanza wa km 42 atapatiwa Sh3 milioni, wakati km 21 atapatiwa Sh2 milioni na mshindi wa kukimbia na baiskeli atapewa Sh2 milioni..
Mbali na Okwi mabalozi wengine wa Tulia Trust ni Mtangazaji wa Clouds, Babra Hassan, msanii wa muziki wa bongo fleva, Lameck Ditto na Nancy
Chanzo: Mwanaspoti