KAMA unadhani aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, amesalimu amri basi utakuwa umekosea sana aisee. Unaambiwa hivi, Wambura ambaye rufani yake kupinga kufungiwa kujihusisha na soka maisha, imetupiliwa mbali na Kamati ya Rufani na Maadili ya TFF, ameapa kuendelea kupambana na kusisitiza kuwa hajakubali.
Jana, Wambura amezungumzia uamuzi wa Kamati ya Wakili Ebenezer Mshana, akisema ulikuwa ni mkakati wa kubariki mtu kuchafuliwa na kusema kamwe hatakubali na anajipanga upya kwa mapambano.
Kauli hiyo ya Wambura inakuja ikiwa ni siku moja tangu Wakili Mshana kutangaza uamuzi wa kamati yake kubariki hukumu ya Wambura kufungiwa maisha iliyotolewa awali na Kamati ya Maadili.
Akitumia dakika 42 kufafanua mambo mbalimbali kuhusiana na uamuzi wa Kamati ya Wakili Mshana, Wambura alisema bado hajapatiwa haki yake ya msingi ya kusikilizwa.
Mdau huyo wa soka, ambaye ana sifa ya kupambana linapokuja suala la kudai haki yake, alisema anasubiri nakala ya hukumu hiyo na baada ya hapo ataketi na timu ya wanasheria wake kuangalia ni mlango sahihi wa kuutumia ili kupata haki yake.
Aliwataka Watanzania na wapenda soka kutulia na kamwe wasiwe na shaka kwa kuwa, anafahamu njia sahihi za kupata haki yake. Pia, amesema kilichofanywa na kamati hizo mbili za TFF ni kutokana na mapambano yake na atatumia shauri hilo kubadili zaidi kanuni za soka la Tanzania ili kila mdau apate haki. “Mpaka sasa haki tunayoipigania hatujaipata kwani, tunataka kupatiwa nafasi ya kusikilizwa na bado tunaona hatujasikilizwa, wanasema wana ushahidi kwanini hawataki tuweke mambo hadharani?,” alihoji Wambura.
“Tuliomba hii kesi isikilizwe kama mahakama ya wazi (open court) hawataki, lakini hukumu yao jana (juzi) wameitoa ikiwa mubashara, tunachotaka Watanzania waone kila kitu ili wawe mashuhuda na kinachoendelea ndani ya TFF,” alisema na kuongeza:
“Wanataka mtu aonekane mwizi, fisadi na wanadai nina kesi ya Simba pale Kisutu wakati ilishafutwa zamani, hilo limetoka wapi. Wamejifungia wenyewe na kutoa uamuzi wa upande mmoja, haiwezekani tutaendelea kutafuta haki yetu mbele. Haya ni mambo ya kimkakati tu.” Awali, Mwanasheria anayemtetea Wambura, Emmanuel Muga alisema ameshangazwa na hatua za kudanganya umma iliyofanywa na kamati hiyo akisema, wamezungumza mambo ya uongo dhidi yake. “Wameamua kwa makusudi kudanganya umma, akisema eti nilimuombea mteja wangu apunguziwe kifungo kitu hicho nawezaje kukifanya kama wakili? “Kuna mambo mengi yamefanyika ambayo kwetu ni kama ulikuwa mpango wa kupunguza haki ya upande mmoja, angalieni walivyobadilisha wajumbe wa kamati siku chache kabla ya kusikilizwa kwa kesi hii, hii kamati haitakiwi kubadilishwa kama walivyofanya,” alisema.
Chanzo: Mwanaspoti