![]() |
Simba yatikisa Msumbiji |
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, wametua salama mjini Beira Msumbiji jana mchana na 'dege' lao la kukodi huku wakiwa na 'fulu muziki' wa kikosi chao cha nyota 19 waliopewa jukumu la kuhakikisha wanarejea na ubingwa nchini.
Simba ambayo jana jioni ilifanya mazoezi mepesi kuelekea mechi yao ya leo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao, UD Songo imepania kufika nusu fainali ya michuano hiyo msimu huu baada ya msimu uliopita kuishia robo fainali.
Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, aliliambia gazeti hili kuwa licha ya muda wa maandalizi kuwa mfupi kutokana na ratiba ya michuano hiyo msimu huu kuanza mapema, ana uhakika wamejiandaa vya kutosha kuweza kufanya vizuri.
Aussems alisema maandalizi waliyoyafanya kambini Afrika Kusini kwa kucheza mechi za kirafiki kabla ya kurejea nchini na kujipima uwezo na Power Dynamos ya Zambia ambapo walishinda 3-1, mechi hizo zimempa nafasi ya kugundua na kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza.
Alisema anatambua mechi hiyo itakuwa ngumu kwa kuwa UD Songo licha ya kuifuatilia na kutuma wawakilishi wake kwenda kuisoma, bado hawezi kuidharau kwa kuwa nayo itakuwa imesajili nyota wapya na baadhi walipumzishwa kwenye mechi waliyokwenda kuishuhudia ikicheza.
Hata hivyo, Aussems ameongozana na kikosi chao chote cha ushindi kilichoshuka dimbani dhidi ya Power Daynamos wakiwamo; Beno Kakolanya, Ally Salim, Gadiel Michael, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Tairone da Silva, Jonas Mkude na Sharaf Shiboub.
Nyota wengine waliopo katika kikosi hicho ni John Bocco, Francis Kahata, Meddie Kagere, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Gerson Veira, Deo Kanda, Rashid Juma na Hassan Dilunga.
Aidha, imewaacha jijini Dar es Salaam, Said Ndemla, Yusuf Mlipili, Kennedy Juma, Aishi Manula, Wilker da Silver, Ibrahim Ajibu, Haruna Shamte na Miraji Athuman.
Katika hatua nyingine, kuelekea kwenye michezo ya kimataifa ambayo inatarajia kuanza kesho kwa timu nne za Tanzania kupeperusha Bendera ya Kimataifa, Uongozi wa Simba umewaangukia mashabiki wao kutozomea wawakilishi wa Taifa.
Mashabiki wa Simba na Yanga wamekuwa na utamaduni mbaya, hasa linapokuja suala la kushangilia kimataifa kwani huwawia vigumu wapinzani hao wa jadi kushangilia mwenzake na badala yake wamekuwa wakiziunga mkono timu pinzani.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema: "Imetuchukua miongo kadhaa kama nchi kupata fursa ya kuwakilishwa na klabu nne kwenye mashindano ya CAF, Simba wana mchango mkubwa sana katika hili.
"Kama Taifa tunatakiwa tufanye vizuri zaidi kupitia wawakilishi wetu ili tuendelee kwa miaka ijayo kuwa na klabu nne kwenye CAF Competitions (michuano ya Caf).
"Najua ni ngumu kunielewa leo , lakini nawaomba Wanasimba wote kesho msizomee @Yangasc, msilipe kisasi na wekeni maslahi mapana ya nchi, sisi ni waungwana na uungwana ni vitendo! Kama hujiwezi usiende Taifa na ikibidi kwenda na huwezi kuwashangilia bora ukae kimya.
"Najua walitukera msimu uliopita, lakini tuiangalie nchi kwanza na pia tujue wao, @azamfcofficial na @kmcfc_official pamoja na sisi ndio tuna nafasi ya kuendelea kupewa nafasi nne tena msimu ujao," alieleza Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram.