![]() |
Harry atua Man United |
Beki huyo kisiki mwenye mwili jumba, jana alikuwa akimalizia mazungumzo ya maslahi yake binafsi baada ya klabu yake na Manchester United kuafikiana ada ya uhamisho ya Pauni 80 milioni, iliyoweka rekodi mpya ya uhamisho wa beki. Imeipiku bei ya Pauni 75 milioni ambayo Liverpool walilipa kwa Southampton ili kumsajili Virgil van Dijk Januari 2018.
Kocha wa Leicester, Brendan Rogers ametoa mkono wa kwaheri kwa beki huyo akithibitisha kuwa klabu hizo mbili zimeshakubaliana ada ya uhamisho, lakini kwa wakati huo maslahi binafsi tu ndiyo yaliyokuwa yakijadiliwa baina ya United na Maguire.
“Ada ya uhamisho imeshaafikiwa," alisema Rogers, "kisha kinachofuata ni suala la Harry kupata nafasi ya kuzungumza nao kuona kama ataafiki malipo binafsi.
"Hilo ni suala la manufaa yake. Na kisha, hakika, atafanyiwa vipimo vya afya. Mbali na hayo sina zaidi la kuongeza.
"Pengine baada ya wikiendi tutajua mengi. Lakini ni wazi timu hizi mbili zilikuwa katika mazungumzo na ada ya uhamisho imeafikiwa.”
Mapema jana taarifa zilivuja kwamba United waliafiki kulipa jumla ya Pauni 80 milioni kwa ajili ya beki huyo mwenye umri wa miaka 26.
Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya England walikuwa wakimfukuzia beki huyo kwa kipindi chote cha dirisha hili la usajili, baada ya awali dili hilo kukwama miezi 12 iliyopita.
Maguire ambaye aliishabikia United utotoni alisema wiki kadhaa zilizopita kuwa amepagawishwa na ofay a kutakiwa na Mashetani Wekundu.