BAADA ya Yanga kutolewa kwenye kinyang'anyiro cha Kombe la Shirikisho (FA Cup), Simba imesema muda umefika wa kuongeza "umakini mno" wakianza na mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji FC leo.
Yanga inayozidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na Simba iliyopo kileleni mwa ligi hiyo, zote zikiwa na pointi 46, juzi ilitolewa katika Kombe la FA na Singida United kwa mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia kumaliza dakika 90, zikitoka sare ya bao 1-1.
Bingwa wa FA, ndiye anayeiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo sasa ili Yanga na Simba ziweze kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, tiketi pekee iliyobaki kwao ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema kuwa hakuna mechi nyepesi kwenye ligi hiyo na wanatarajia kupata ushindani kutoka kwa Njombe Mji kwa sababu wao pia wanataka kujinusuru na janga la kushuka daraja.
Djuma alisema wamewataka wachezaji wao kuwaheshimu Njombe Mji na kutoshuka uwanjani huku wakikumbuka matokeo ya mechi yao iliyopita ambayo walishinda mabao 4-0.
"Ushindani wa ubingwa upo pale pale, ila sasa tunahitaji umakini mno. Lakini kila mechi ina programu yake na ina mbinu zake, ninawaambia wachezaji tuko vitani na ubingwa hauna mwenyewe, tunatakiwa tuendelee kuongoza mpaka mwisho na hapo tutafanikiwa, hatutakata tamaa, kila mmoja anataka mafanikio," alisema kocha huyo wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda.
Naye Daktari wa Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, Yassin Gembe, alisema jana kuwa kiungo wa timu hiyo, Jonas Mkude, ambaye alipata majeraha wiki iliyopita hali yake inaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi na wenzake.
"Hali yake imeimarika, anaendelea vyema na nimemruhusu kuanza mazoezi, kucheza au kutokucheza kuko chini ya mamlaka ya kocha mkuu, " alisema kwa kifupi daktari huyo.
Mlage Kabange, Kocha Mkuu wa Njombe Mji aliliambia gazeti hili kuwa wanawaheshimu wapinzani wao Simba na wanaamini mchezo wa leo utakuwa na ushindani mkali.
"Kila timu inashuka ikiwa na malengo yake na tuko kwenye vita tofauti, atakayeshinda atakuwa ameendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kufikia malengo yake, kwa upande wetu hatujakata tamaa, nafasi ya kubaki Ligi Kuu bado tunayo, tuombeeni tufanye vizuri mechi zilizobakia," alisema Kabange.
Chanzo: IPP Media